Wednesday, December 3, 2014

Balozi Seif Ali Idd aweka wazi CCM imejipanga kudhibiti wenye nia ya kuvuruga uchaguzi mkuu ujao

948

Mlezi wa CCM Mkoa wa Magharibi Balozi Seif akimkabidhi kadi mwanachama Thuwaiba Jeni Pandu akiwa miongoni mwa wanachama wapya wa CCM na Jumuia zake kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Tawi la CCM Pangawe Jimbo la Fuoni.
Na Othman Khamis Ame.
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
 Mlezi wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Magharibi ambae pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif Ali Iddi, amewahakikishia wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwamba uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka 2015 unatarajiwa kuwa wa utulivu na amani.
Amesema serikali kupitia vyombo vyake vya dola itahakikisha kuwa vikundi vya kihuni vinavyoanza kuandaliwa kwa ajili ya kuvuruga uchaguzi huo vinathibitiwa kwa nguvu zote.
Balozi Seif ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameeleza hayo wakati akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Kwamabata Magogoni, baada ya kumaliza ziara ya siku mbili ndani ya  Mkoa wa Magharibi akiwa mlezi wa CCM Mkoa wa huo.
Amewaomba wafuasi wa vyama vya upinzani hapa Nchini kuamua mapema kufuata chama chenye muelekeo wa kuleta maendeleo ya wananchi, ambacho kwa hivi sasa ni chama cha Mapinduzi.
950
Wanachama wapya 50 wa Chama cha Mapinduzi na Jumuia zake wa Jimbo Jimbo la Fuoni wakila kiapo cha utii baada ya kukabidhiwa kadi kwenye mkutano wa hadhara hapo Tawi la CCM Pangawe.
Amefahamisha kwamba ushindi wa chama cha mapinduzi mwaka 2015 hauna mbadala kutokana na ilivyojipanga na kuungwa mkono na wananchi walio wengi hapa Nchini.
Balozi Seif Ali Iddi amewatahadharisha wana CCM na wananchi  wote kujiepusha na wimbi la vikundi vilivyokubali kujiingiza katika vitendo vya ugaidi ambayo kamwe havikubaliki kitaifa wala kimataifa.
Amesema serikali zote mbili kupitia vyombo vyote vya dola zitakuwa makini kufuatilia mienendo ya watu hao na kuwashughulikia kwa mujibu wa sheria zilizopo.
900
Vijana wa matambuizo wa Umoja wa Vijana wa CCM Jimbo la Mtoni wakifanya vitu vyao wakati wa mkutano wao na Mlezi wa Mkoa wa Magharibi Balozi Seif aliyefanya ziara kukagua maendeleo ya Chama Mkoani humo.
Katika Mkutano huo wa hadhara Balozi Seif ambae pia ni Naibu Kamanda wa Taifa wa Umoja wa Vijana wa CCM Tanzania amewatawadha makamanda wa Vijana wa Majimbo na Wilaya zilizomo Mkoa wa Magharibi Kichama baada ya kuteuliwa na Baraza Kuu la UVCCM.
Makamanda hao ni Mh. Thuwaiba Kisasi Kamanda wa Mkoa wa Magharibi, Kanal mstaafu Masoud Khamis Wilaya, Ibrahim Ramadhan Jimbo la Mtoni, Fatma Adam Jimbo la Bububu, Bimkubwa Nassor Jimbo la Mfenesini, Ibrahim Raza Jimbo la Dimani, Hafidh Tahir Ali Jimbo la Fuoni, Ahmada Abdullwakil Jimbo la Mwanakwerekwe na Abass Hassan Juma Jimbo la Magogoni.
894
Mlezi wa CCM Mkoa wa Magharibi Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akikagua Jengo la Kituo cha Afya cha Jimbo la Mtoni ambalo lililoanzishwa kwa mchango wa Wananchi na Viongozi waliopita wa jimbo hilo.(Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ).

No comments:

Post a Comment