Wednesday, 10 December 2014
Mapya kuhusu ESCROW, Shule ya Prof Tibaijuka yathibitisha kupokea pesa' in good faith'

TAARIFA YA BODI YA WADHAMINI WA JOHA TRUST KWA WAZAZI NA UMMA KUHUSU MCHANGO WA SHS BILIONI 1.617 KUTOKA KWA BW. JAMES RUGEMALIRA WA TAREHE 12 FEBRUARI, 2014
1. Bodi ya Wadhamini ya Shirika la Barbro Johansson Girls’ Education Trust
(JOHA TRUST au BARBRO) inatoa taarifa hii kutokana na utata
uliojitokeza kuhusu mchango wa Shs bilioni moja milioni mia sita kumi na
saba na lhaki moja (Shs 1,617,100,0000/- ) tulioupokea kutoka kwa Bw
James Rugemalira wa VIP Engineering and Marketing Limited.
2.
Mwanzilishi wa Shirika na Malengo yake: Bodi ya Wadhamini BARBRO
inachukua nafasi hii kufafanua kwamba kiongozi wa Waanzilishi wa asasi
yetu ni Mhe Profesa Anna Tibaijuka ambaye pia ni Waziri wa Ardhi, Nyumba
na Maendeleo ya Makazi. Malengo na madhumuni ya taasisi ya JOHA TRUST
ni kuendeleza elimu kwa mtoto wa kike kwa kuwafadhili wasichana wenye
vipaji lakini watokao katika familia za kipato kidogo kusoma katika
shule bora inazoziendesha.
3. Jina la taasisi ya JOHA TRUST linatokana na uamuzi wa wanawake waanzilishi kumpa heshima Hayati Dr. Mama Barbro Johansson (1912-1999) aliyewasili kutoka Sweden
mwaka 1946 kama mmisionari na kuanzisha shule ya wasichana ya kati hapo
Kashasha Bukoba. Mwaka 1954 alijiunga na Mwalimu Nyerere kupigania
uhuru na baadaye kuwa raia wa Tanzania na Mbunge. Mwaka 1964 aliombwa na Mwalimu Nyerere kujitolea kuwa Mwalimu Mkuu wa sekondari ya juu (High School)
pekee ya wasichana ya Tabora Girls iliyokuwa imekumbwa na utovu wa
nidhamu na kutaka kufungwa. Mama Barbro akafanikiwa sana kuigeuza shule
hiyo kiasi kwamba ilipata nishani ya UNESCO mwaka 1967. Mama Barbro
ndiye alianzisha elimu ya watu wazima nchini na pia ndiye alimuunganisha
Mwalimu Nyerere na wahisani kutoka nchi za Nordic ambazo zilianza
ufadhili wake katika Kituo cha Elimu Kibaha na Kituo cha Kilimo, Uyole,
Mbeya.
4. Shule za JOHA
TRUST na Sura yake: Shirika linamiliki na kuendesha Sekondari mbili
nchini. Kwanza ni Sekondari Bingwa ya Barbro iliyopo jijini Dar es
Salaam. Ilianzishwa mwaka 2000 ikiwa na wasichana 40 na hivi sasa wapo
632 wote wa bweni katika kidato cha 1 hadi 6. Pili ni Kajumulo Girls’
High School iliyopo Manispaa ya Bukoba. Ilianzishwa mwaka 2010 ikiwa na
wasichana 31 na hivi sasa wapo 151 katika kidato cha 1, 5 na 6. Jumla
shule hizi zina wanafunzi 783 na waliomaliza ni 1,512. Wote isipokuwa 5
walifaulu mitihani na kujiunga na elimu ya juu katika vyuo vikuu mbali
mbali ndani na nje ya nchi.
Kwa kulingana na uwezo wa mfuko wa ufadhili, wasichana 453 sawa na
asilimia 30% ya wanafunzi wamesaidiwa karo. Shule ya Barbro imekuwa
miongoni mwa shule kumi bora Tanzania (2010) na kwa wastani inakuwa kati
ya shule 50 bora katika mitihani ya taifa. Itambulike kwamba mafanikio
haya yanapatikana pamoja na shule kuwa na sera
ya kutowafukuza wanafunzi kwa misingi ya ufaulu wa mitihani ili mradi
wawe na nidhamu. Falsafa yetu ni kuwahimiza wanafunzi kuweka bidii kadri
ya uwezo wao, kujithamini na kujiamini katika maeneo wanayofanya
vizuri. Kipa umbele chetu
ni maendeleo ya mwanafunzi mmoja mmoja kwanza na sifa kwa shule
baadaye. Katika hali hii walimu hawana budi kufanya kazi ya ziada.
5.
Gharama za Uendeshaji na vyanzo vyake: Tangu ianzishwe JOHA TRUST
imetumia gharama ya Shs bilioni thelathini na mbili (Shs
32,267,000,000/-) ambazo zimetokana na karo na michango ya wazazi
asilimia 37%; wafadhili wa nje asilimia 35%, wafadhili wa ndani asilimia
7% na mikopo asilimia 21%. Kama taasisi nyingi zinazotoa elimu, JOHA
TRUST inakabiliwa na uhaba wa fedha na ujenzi bado kukamilika. Shule
inatoa huduma ya elimu bora na haifanyi biashara kama wengi wasioelewa
wanavyofikiri. Bila ruzuku na misaada viwango vyake vya juu
haviwezekani. Shirika la misaada la Sweden (SIDA ) ambalo limekuwa
mfadhili mkubwa limekamilisha ahadi yake ya ufadhili wa miaka 10
(2002-2012) lililopanga kwamba ingelitosha kusimika taasisi ya JOHA
TRUST na kuitaka ijitegemee. Hata hivyo SIDA imeacha utekelezaji wa
Master Plan ya BARBRO ya mwaka 2004 bado kukamilika. Jambo hili limekuwa
changamoto kubwa kwa Bodi kwa sababu katika Master Plan SIDA
ilipandisha viwango vya majengo kuwa juu kulingana na sifa na hadhi ya
Mama Barbro. Ikihitimisha ufadhili huo, SIDA ilihimiza Bodi kuhamasisha
michango ya ndani ili kujenga uendelevu na kukamilisha ujenzi wa Master
Plan hiyo.
6.
Maombi ya Ufadhili: Kwa kuzingatia ushauri huo wa SIDA, mwaka 2012 Bodi
ilimtaka Mwanzilishi (ProfesaTibaijuka) ambaye pia ni Mtafuta Fedha
(Fund Raiser) wa JOHA TRUST kuwaomba baadhi ya wafanyabiashara mashuhuri
nchini kuunga mkono shughuli za asasi yetu kwa michango. Bwana na Bibi
James Rugemalira ni miongoni mwa wafanyabiashara walioombwa mchango huo
kwa barua ya tarehe 4 Aprili 2012 kupitia kampuni yao ya Mabibo Beer
Wines and Spirits Limited. Hatimaye mapema Februari 2014, bila kutaja ni
kiasi gani, Bw. Rugemalira alimjulisha Mwanzilishi kwamba yuko tayari
kufanya mchango ulioombwa na kumwagiza kwamba sharti
ni yeye Mwanzilishi kufungua account hapo Mkombozi Benki kuupokea
mchango huo na kuchukua jukumu la kuufikisha shuleni na kuhakikisha
unatumika kama ilivyokusudiwa. Bw Rugemalira alieleza hakutaka
kuhangaika kuhamisha fedha kwenda benki nyingine ambapo tayari kulikuwa
na akaunti za shule.
7.
Mchango wa VIP ulivyopokelewa: Kama alivyotakiwa, Mwanzilishi alifungua
account hiyo hapo Benki ya Mkombozi tarehe 3 Februari, 2014 na kuupokea
mchango huo wa jumla ya bilioni moja, milioni mia sita kumi na saba na
lhaki moja (Shs 1,617,100,000/=) kwa niaba ya shule tarehe 12 Februari,
2014 kutoka kwa kampuni ya VIP Engineering and Marketing.
8.
Maamuzi ya Bodi: Bodi ya Wadhamini BARBRO ilikaa katika kikao maalum
tarehe 13 Februari, 2014 kupokea taarifa ya mchango huo mkubwa kutoka
kwa Bw. Rugemalira kupitia kampuni yake ya VIP Engineering. Bodi
iliukubali na kuamua mchango huo utumike kulipa sehemu ya deni la shule
hapo Bank M ambalo lilikuwa changamoto kubwa. Kwa hiyo Mwanzilishi
aliagizwa na Bodi kuhamisha fedha hizo kutoka akaunti yake ya Mkombozi
kwenda akaunti ya Bank M kulipia mkopo huo. Hii inafafanua kwa nini
fedha zilihama kwa haraka kutoka Benki ya Mkombozi kwenda Bank M kwa
wale wanaohoji suala hili.
9.
Ulipaji wa Deni na Madai yaliyobakia: Ili kutekeleza Master Plan, Julai
2011 JOHA TRUST ilikuwa imechukua mkopo wa Shs bilioni mbili (Shs
2,000,000,000/-) hapo Bank M kwa ajili ya ujenzi wa bweni kubwa lenye
uwezo wa vitanda 163. Hadi kufikia tarehe 19/04/2014 mkopo huo
ulipolipwa wote, deni hilo lilikuwa limezaa riba na gharama nyingine na
kuongezeka hadi kufikia takriban jumla ya Shs bilioni mbili, milioni mia
saba arobaini na moja, lhaki tatu sabini na nne elfu, mia nne arobaini
na nne (Shs 2,741,374,444/-). Kwa hiyo, pamoja na ukubwa wa mchango wa
Bw Rugemalira bado umelipia sehemu ya deni hilo tu. Sehemu nyingine
iliyobaki (Shs 1,124,274,444/-) imelipwa kutoka vyanzo vingine vya
mapato ikiwemo mkopo wa milioni mia mbili tisini na moja, lhaki tatu
sabini na nne, mia nne arobaini na nne (Shs 291,374,444/-) zilizotolewa
na Mwanzilishi kulipa riba ya kila mwezi wakati wa uhai wa mkopo huo.
Ilikuwa maamuzi ya Bodi kupunguza madai hayo ya Mwanzilishi kutoka
takriban Shs milioni 291 na kubakia takriban Shs milioni 174 . Kwa hiyo
fedha zote alizozitoa Bw Rugemalira za Shs 1.617,100,000/- zilitumika
kulipa mkopo na wala hazikutosha. Katika hali hiyo, hisia na madai
yanayotolewa kwamba Mwanzilishi alijinufaisha na fedha hizo SI KWELI.
Isingewezekana.
10. Ufadhili Endelevu wa Shule: Itambulike kwamba hata kwa nafasi yake
Mwanzilishi ni mfadhili na mdhamini mkubwa wa JOHA TRUST kwa fedha zake
binafsi. Bodi ilimwomba awe analikopesha shirika letu na wafadhili
wakipatikana tunamrejeshea fedha
zake polepole. Kwa mfano SIDA iliwahi kuridhia kwamba sehemu ya msaada
wake utumike kurejesha mkopo uliotolewa na Mwanzilishi wakati wa
kuanzisha shule kati ya mwaka 2000 hadi 2003.
11.
Mchango wa VIP ulipokelewa kwa nia Njema. Shirika halina utaratibu
kuwahoji wafadhili wetu wa ndani au nje kwanza kuthibitisha chanzo cha
fedha zao wanazotuchangia. Misaada na michango, iwe mikubwa au midogo,
yote imekuwa ikipokelewa kwa nia njema tukiamini pia inatolewa kwa nia
njema. Tunaamini hivi pia ndivyo ilivyo kwa asasi nyingine nchini na
jamii kwa ujumla kwa mfano michango ya maendeleo na hata harusi na
shughuli nyingine kama hizo. Kwa kuwa tulihakikishiwa na Benki ya
Mkombozi kwamba fedha za Bw Rugemalira zilikuwa zimelipiwa kodi,
tulipokea mchango wake kwa furaha bila wasi wasi wowote.
12. Michango ya kuendeleza shule siyo zawadi binafsi kwa viongozi wake: Tunatambua kuwa sheria ya Maadili
ya viongozi huwataka kuwasilisha zawadi zote zinazozidi Shs elfu
hamsini (Shs50,000/-) kwa mwajiri wao. Kuna wanaodai Mwanzilishi
amekiuka maadili kwa kutouwasilisha mchango huo Serikalini. Pia kuna
wanaohoji kwa nini mchango mkubwa huo haukwenda kwenye jimbo lake la
uchaguzi (Muleba Kusini) ili kuendeleza shule za Kata. Wote wanakosea.
Mchango ulitolewa kwa shule ya JOHA TRUST na Mwanzilishi alipoufikisha
kwetu tuliupokea na kuutumia kama ilivyokusudiwa kwa shughuli za
maendeleo ya shule na kumwendeleza mtoto wa kike. Kufanya vinginevyo
ndiko kungelikuwa kukiuka maadili.
13.
Umuhimu wa Uchunguzi: Kupitia luninga tulifuatilia mjadala Bungeni
Dodoma jioni ya Ijumaa tarehe 28, Novemba, 2014 kabla ya kikao hicho
kuvurugika. Tulishuhudia jinsi Bunge zima lilivyoazimia kwamba vyombo
vya uchunguzi vifanye kazi yake kuhusu waliopata ͞mgao͟ ili kuondoa
mashaka na taarifa kamili zipatikane ili pale penye makosa hatua stahiki
kuchukuliwa. Kwa hiyo, katika kikao cha Bodi cha tarehe 2 Desemba,
2014, kilichoitishwa rasmi kujadili jambo hili, kwa kauli moja tunatamka
kwamba hatuamini kabisa na tunashindwa kuelewa kwa nini Mwanzilishi
wetu atakiwe kuwajibishwa nafasi yake Serikalini kwa kuwa tu alipokea
mchango wa shule kwa niaba yetu. Jambo hili litatuchanganya na
kutukatisha tama sisi wananchi wa kawaida tunaojitolea kutekeleza
shughuli mbali mbali za maendeleo hususan elimu. Tunaamini hatua hiyo
pia itafifisha juhudi za viongozi wengine wengi wanaohangaika
kuhamasisha michango ya shughuli mbali mbali za maendeleo ikiwemo elimu,
afya, maji, vijana, walemavu, watoto yatima, watoto wanaoishi kwenye
mazingira hatarishi, wazee, wajane, n.k. katika taifa letu changa.
Tunaomba Mhe Rais alione jambo hili. Ikiwa michango ya maendeleo
inayopokelewa na viongozi kwa niaba ya wadau wao itatafsiriwa kama
zawadi zao binafsi kuna hatari kuzorotesha ͞harambee͟ za maendeleo.
Tunaamini ufafanuzi huu utatosha kuondoa utata katika suala hili ili
umma na viongozi wa ngazi za juu wapate ukweli juu ya jambo hili na
ushiriki wetu. Bodi yetu iko tayari kujibu maswali yoyote yanayoweza
kuulizwa ili kuondoa utata huu kabisa.
14.
Shukrani kwa Wafadhili: Katika miaka 15 ya uwepo wa taasisi yetu (2000
-2014) , JOHA TRUST imepokea michango jumla ya Shs bilioni 13.59 kutoka
kwa wafadhili mbalimbali. Wafadhili wakubwa wa nje ni SIDA ambayo imetoa
jumla ya Shs bilioni 8. 15 sawa na asilimia 60% na JOHA TRUST Sweden
Shs bilioni 1.79 sawa na asilimia 13.11%. Mwaka 2000 Serikali ya
Tanzania chini ya Mhe Rais mstaafu Benjamin Mkapa ilitoa ardhi ekari 50
kujenga shule ya Barbro jijini Dar es Salaam. Mwaka 2005 kabla ya
kuondoka madarakani Rais Mkapa alikuja kama mgeni rasmi kwenye mahafali
ya kidato cha nne kukagua maendeleo yetu, akaridhika na kuchangia Shs
milioni tano (Shs 5,000,000/-). Kwa wahisani wa ndani ya nchi Dr.
Reginald Mengi Mwenyekiti wa IPP amechangia jumla ya Shs milioni 278
mwaka 2013 alipokuwa mgeni rasmi kwenye mahafali ya kidato cha nne. Kwa
hiyo alichofanya Bw James Rugemalira ni sawa sawa na wahisani wengine
waliotuunga mkono. Tunawashukuru wafadhili wetu wote wa ndani na nje ya
nchi kwa michango yao na tunawaahidi kuongeza juhudi zetu za
kumwelimisha mtoto wa kike na kwa kufanya hivyo jamii nzima ya
Watanzania.
15.
Ujumbe kwa Wazazi: Kama ilivyofafanuliwa tarehe 25 Septemba, 2014
katika mahafali ya kidato cha nne, ni muhimu kwa wazazi na walezi
kuyaelewa vizuri yaliyojiri katika suala hili kuepuka upotoshwaji
unaotokana na sababu za kisiasa dhidi ya Mwanzilishi wetu. Pamoja na
matatizo yaliyojitokeza hatujakata tamaa katika juhudi zetu kumjengea
uwezo mtoto wa kike. Tunawaahidi wazazi ambao wamekuwa na wasiwasi
kuhusu ufadhili wa watoto wao kwamba kazi inaendelea kama kawaida. Hivi
sasa wasichana 83 katika shule ya BARBRO na wasichana 20 katika shule ya
KAJUMULO wanasoma kwa ufadhili. Tunawahakikishia wasichana wote hawa
103 ambao ni asilimia 13% ya wanafunzi wote 783 tulionao wasiwe na
wasiwasi bali kuendelea kusoma kwa bidii. Hakuna binti mwenye ufadhili
tayari atakayepoteza nafasi yake katika shule zetu kwa sababu ya tukio
hili. Tunachukua nafasi hii kuhimiza michango kutoka kwa wafadhili
wengine watakaoguswa na juhudi zetu ili tuweze kuongeza uwezo wa
kuwafadhili wahitaji wafikie asilimia 30% tuliyokusudia. Pamoja
tuendelee kushirikiana katika kuendeleza elimu na ulezi bora kwa mtoto
wa kike. Kama alivyosema Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere ͞Hasa wakati wa
shida kukata tamaa ni dhambi
No comments:
Post a Comment