UJENZI WA MABWENI SHULE ZA PEMBEZONI KUPUNGUZA MSONGAMANO WA WANAFUNZI MIJINI.
Na. Aron Msigwa – MAELEZO.
Jamii imetakiwa kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali za ujenzi wa mabweni katika shule za Sekondari zilizoko
pembezoni mwa miji hasa maeneo ya vijijini ili kukabiliana na tatizo la
msongamano wa wanafunzi mijini linalosababishwa na baadhi ya wanafunzi
kushindwa kujaza nafasi wanazopangiwa maeneo ya pembezoni mwa miji kutokana na umbali.
Kauli
hiyo ilitolewa juzi jijini Dar es salaam na Katibu Tawala wa mkoa wa
Dar es salaam Bi. Theresia Mmbando wakati akizungumza na viongozi wa
Elimu wa mkoa na walimu wakuu wa Shule za Sekondari za mkoa wa Dar es
salaam wakati wa kikao cha Kamati ya Uchaguzi wa wanafunzi wa
watakaojiunga na kidato cha kwanza mwaka 2015.
Alisema
mwaka huu mkoa wa Dar es salaam umekuwa na kiwango cha juu cha
ufaulu kitaifa kwa kuwa na wanafunzi wanaokidhi vigezo vya kuendelea na
masomo ya sekondari kwa kiwango cha asilimia 78 ukifuatiwa na mkoa wa
Kilimanjaro ambao umepata asilimia 69.
Alifafanua
kuwa kati ya wanafunzi 60,709 waliosajiliwa kufanya mtihani wa kumaliza
Elimu ya Msingi mwaka huu , wanafunzi 59,577 ambao ni sawa na asilimia
98.14 waliofanya mtihani huo, wavulana wakiwa 28,419 na wasichana
31,158.
Bi.
Mmbando alibainisha kuwa kati ya hao watahiniwa 1,132 sawa na
asilimia 1.86 katika mkoa wa Dar es salaam hawawakuweza kufanya mtihani
huo kutokana sababu mbalimbali zikiwemo utoro, vifo, ugonjwa na sababu
nyinginezo.
Akizungumzia
kuhusu ufaulu wa wanafunzi hao kimkoa alisema wanafunzi 46,434 sawa na
asilimia 78 walifaulu mtihani huo na kuufanya mkoa wa Dar es salaam
kuongoza kwa kuwa na ufaulu wa juu kitaifa wavulana 22,389 na wasichana
24,086.
Alibainisha
kuwa wanafunzi 36,610 walichaguliwa katika chaguo la kwanza kujiunga na
shule mbalimbali za Sekondari za ndani na nje ya mkoa wa Dar es salaam
na kufafanua kuwa wanafunzi 9824 waliobaki sawa na asilimia 21 ambao nao
wamefaulu watachaguliwa katika chaguo la pili kufuatia baadhi ya
wanafunzi waliochaguliwa katika chaguo la kwanza kujiunga na shule
zisizokuwa za serikali na nafasi zao kubaki wazi.
Katika
kufanikisha zoezi hilo Bi. Mmbando alieleza kuwa mkoa tayari umeunda
timu tatu zitakazofuatilia idadi ya wanafunzi watakaoshindwa kufika
katika shule walizopangiwa kuanzia Januari 14, 2015 katika halimashauri
za Temeke, Ilala na Kinondoni ili nafasi zao zijazwe na wanafunzi
wengine.
Kwa
upande wake Afisa Elimu wa Mkoa wa Dar es salaam Bw. Raymond Mapunda
akitoa tathmini ya mtihani wa kumaliza Elimu ya Msingi uliofanyika nchi
nzima mwezi Septemba mwaka huu alisema mkoa wake ulifanya vizuri
kutokana na juhudi za walimu pamoja na wanafunzi kuuelewa vizuri mfumo
wa ufanyaji mitihani uliotumika wa Optical Mark Reader (OMR).
Alisema
kuwa wanafunzi wa shule 506 za jiji la Dar es salaam walifanya mtihani
walitumia mfumo huo kwa ufanisi mwanafunzi 1 alifutiwa matokeo yake kwa
sababu za udanganyifu, 2 walipata alama 0 huku wavulana 10 na
wasichana 10 kutoka wilaya ya Ilala na Kinondoni waliibuka washindi wa
nafasi 10 bora kitaifa.
No comments:
Post a Comment