

Wananchi wengi walikwazwa na hali hiyo, kwani
wakati baadhi ya viongozi walisema uchaguzi huo ungeahirishwa hadi
mapema mwakani, wengine walisema ungefanyika pamoja na Uchaguzi Mkuu
mwishoni mwa mwaka ujao.
Wananchi walikwazwa na mkanganyiko huo kutokana na
ukweli kwamba Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ni muhimu mno, pengine
kuliko uchaguzi mkuu wa nchi yoyote, kwani ndiyo hasa hutoa sura na
taswira ya mamlaka ya wananchi walio wengi kuanzia ngazi za chini ambako
ndiko viongozi katika ngazi zote nchini hupata uhalali wa kuongoza. Kwa
maana hiyo, uchaguzi huo ni muhimu katika kudumisha demokrasia na
utawala bora katika nchi. Ndiyo maana serikali nyingi duniani huelekeza
nguvu na rasilimali nyingi katika kuhakikisha kwamba uchaguzi wa
serikali za mitaa unafanyika na unakuwa huru na haki. Licha ya gharama
kubwa, uchaguzi huo huhitaji muda wa kutosha kuhamasisha wananchi
wajitokeze kupiga kura siku ya uchaguzi ili kuunda serikali ambayo
itashughulikia matatizo ya wananchi katika ngazi hiyo muhimu.
Pamoja na kutangaza tarehe za kujiandikisha na
kupiga kura, Serikali haionekani kama imefanya maandalizi ya kutosha
kufanikisha uchaguzi huo. Wananchi, wakiwamo viongozi wa vyama vya
siasa, wanahoji kwa nini haujafanyika uhamasishaji wa kutosha kwa
wananchi ili wajiandikishe na kushiriki kikamilifu kugombea nafasi za
uongozi au kuwachagua viongozi wanaofaa kuwaongoza. Wanasema haitoshi
kwa Serikali kutaja gharama za kuendesha uchaguzi huo, bila kuhakikisha
kwamba wagombea na wananchi kwa jumla wanafahamu taratibu na kanuni za
uchaguzi huo, ikiwa ni pamoja na vituo vya kujiandikisha, kupigia kura,
wasimamizi, wajibu na nafasi ya mawakala wa vyama vya siasa na sifa za
wagombea na wapigakura.
Ikiwa zimebakia siku saba tu kabla ya kuanza
uandikishaji wa wapigakura, mazingira yaliyopo hivi sasa hayaonyeshi
ujio wa tukio kubwa kama hilo. Hivyo uwezekano wa wananchi wengi
kutojiandikisha kupiga kura ni mkubwa. Tungetarajia ‘habari ya mjini’
hivi sasa iwe ni uchaguzi huo, lakini kinyume chake mazungumzo nchi
nzima yameelekezwa kwenye mambo mengine, ikiwa ni pamoja na suala la
akaunti ya Tegeta Escrow.
Pamoja na Serikali kuchelewa kuchukua hatua
stahiki na kuupa uchaguzi huo kipaumbele, tunadhani inaweza kutumia muda
mfupi uliobaki kuelekeza nguvu na rasilimali zake katika kuhakikisha
kwamba uchaguzi huo unafanyika kwa mafanikio makubwa, hasa kwa
kuzingatia kwamba dhumuni la kuwapo Serikali za Mitaa ni kupeleka
madaraka kwa wananchi ambao ndio chimbuko la mamlaka yote katika nchi
yetu.
Tunaishauri Serikali iondoe kasoro
zinazolalamikiwa, ikiwa ni pamoja na mkanganyiko katika mwongozo na
baadhi ya kanuni za uchaguzi huo. Vinginevyo uchaguzi huo utagubikwa na
sintofahamu na kusababisha vurugu ambazo zingeweza kuepukwa. Ni jukumu
la kila mmoja wetu kuhakikisha uchaguzi huo unakuwa huru na wa haki,
kwani kufanya hivyo kutasimika misingi ya utawala bora katika ngazi
mbalimbali, kuanzia serikali za mitaa.
chin
No comments:
Post a Comment