Raila Odinga vs Uhuru Kenyatta
Mwanzoni mwa miaka 1980 Jaramogi Oginga Odinga alikuwa katika wakati
mzuri kujifufua kisiasa na akatumia nafasi ya kisiasa kumsimanga rais wa
kwanza wa Kenya Jomo Kenyatta kama mkwapuaji wa ardhi. Leo hii Raila
Odinga, mtoto wake anayegombea urais wa Kenya kwa Muungano wa Mageuzi na
Demokrasia - CORD naye anatumia kibwagizo cha baba yake kwa kusema kuwa
Uhuru Kenyatta, mgombea wa Muungano wa Jubilee ni mkwapuaji ardhi.
Ukitizama historia ya Kenya, baada ya kifo cha rais Jomo Kenyatta na
Rais Daniel Arap Moi kuchukua nafasi yake mwaka 1978, alijaribu
kuhakikisha wapigania uhuru wote ambao walihitilafiana na hayati rais
Kenyatta anawarudisha serikalini na kuwapa vyeo katika kujaribu kujenga
umoja wa kitaifa. Oginga Odinga aliteuliwa kuwa mwenyekiti wa bodi ya
Pamba ambayo ilimuwezesha kurudia harakati zake za kisiasa.
Siku moja alihutubia mkutano wa hadhara aliamua aeleze ni kwanini
alikosana na Hayati Kenyatta na akasema sababu kubwa ilikuwa eti rais
Kenyatta alikuwa rais aliyekuwa anatetea wachache matajiri wakati yeye
alikuwa anaamini katika falsafa ya fursa sawa katika kumiliki ardhi na
kuwapa upendeleo maalum kwa masikini wanaohitaji ardhi. Baada ya Oginga
Odinga kuueleza umma ni kwanini alikosana na hayati Kenyatta, rais
Daniel Arap Moi alichukizwa na kauli zake na mara moja aliagizwa
akamatwe tena na akawekwa kizuizini hadi miaka ya 1990 wakati harakati
za demokrasia ya vyama vingi ziliposhika kasi.
Kinachotokea kwa sasa nchini Kenya ni marudio ya enzi ambapo watoto wa
Kenyatta na Oginga Odinga wanachuana katika kupata madaraka katika
uchaguzi wa mwezi ujao. Suala la ardhi limejitokeza kuteka vichwa vya
habari hasa pale Raila Odinga wakati akizindua kampeni zake za kisiasa
alikumbushia kuwa familia ya Uhuru Kenyatta inamiliki ardhi kubwa ya
ukubwa wa eneo zima la Jimbo la Nyanza. Katika kujaribu kujisafisha,
Uhuru Kenyatta aliwambia watu katika kampeni zake kuwa kama kuna mtu ana
ushahidi wa ukwapuaji wa ardhi uliofanywa nay eye akamshtaki
mahakamani. Na akaongezea kuwa yeye si mkwapuaji ardhi ila Raila Odinga
lazima ajibu tuhuma za kukwapua kiwanda cha molasses (sukari guru) huko
Kisumu.
WELEDI WA WAGOMBEA WA KISIASA
Kimsingi, Raila Odinga ameamua kutumia suala la ardhi kama eneo lenye
udhaifu kwa weledi wa Uhuru Kenyatta. Nikumbushe kuwa hakuna mtu amewahi
kupima na kujua ukubwa wa ardhi inayomilikwa na familia ya Kenyatta.
Lakini inachukuliwa kama ni ukweli usiopingika kuwa ardhi ya familia ya
Kenyatta inasemekana inaanzia Pwani ya Kenya hadi kukutana na Jimbo la
Bonde la Ufa. Uhuru wa Kenyatta anabakia kuwa kama mtu anayeishi kwa
kufaidi matunda yaliyokwapuliwa na baba yake; lakini tujiulize je ni
sahihi kwa mtoto kulipa dhambi zilizofanywa na baba yake?
Kama watanzani ni vyema tujifunze kitu kutokana na yanayotokea nchini
Kenya kwa sasa. Ardhi ni jambo la kuangaliwa kwa umakini sana duniani
kote. Ninaiona hizi kukashifiana kati ya Kenyatta na Odinga kama kukosa
busara na ni aina ya ubaguzi wa kisiasa uliojaa unafiki wa hali ya juu
(disingenuous).
Ukifuatilia siasa za Kenya ni nchi ambayo ilichagua kufuata sera za
kibepari ambazo zinazingatia umiliki binafsi wa mali (private ownership)
na wala si umilikaji mali kwa pamoja (collectivism). Ubepari ni mfumo
uliojaa kutokujali haki, usawa,na kushadidia utendaji wa kutokujali
taratibu.
Kwa kuzingatia sera za kibepari, ardhi ikishanyakuliwa hairudi tena.
Ukisoma historia, kwa mfano, wakati wavamizi kutoka uingereza
waliponyakua ardhi za wenyeji wa Amerika kule Manhattan ndio ilipotea
kabisa na walionyakuwa wakaiendeleza. Raila Odinga anachofanya ni
kujaribu kupata umaarufu wa kisiasa (cheap politics) na wote wawili ni
kielelezo cha siasa za hovyo za kiafrika. Raila Odinga anachotukumbusha
ni kuwa sasa ni wakati kwa Uhuru Kenyatta kuona ukwapuaji wa ardhi
uliofanywa na baba yake anaurekebisha kwa kuwarudishia ardhi hiyo wale
ambao hawana ardhi na walifukuzwa maeneo hayo wakati huo wa ukoloni.
Ni jukumu la wanasiasa wa leo kutuonesha kuwa dhambi za tawala za
zamani zifutwe na zisiendelezwe tena kipindi cha sasa.
Yaani anamaanisha eti Uhuru Kenyatta anapaswa kutumia kampeni hizi
kuwaahidi wakenya ambao walifukuzwa kwenye ardhi zao na kunyakuliwa na
baba yake Mzee Kenyatta kuwa atawarudishia kiasi fulani cha ardhi ambayo
baba yake alitumia madaraka vibaya kwa kuamua kujimegea ardhi kutoka
kwa wakoloni wa kiingereza na kutowarudishia walionyang’anywa yaani
Wakenya wenzake.
WANASIASA NI WAONGO
Kimsingi, Uhuru Kenyatta alikuwa na umri mdogo sana wa miaka 15 wakati
Mzee Kenyatta anafariki dunia. Kusema yeye ndiye aliyerithi ardhi ya
baba yake ni makosa; ila ardhi hiyo ilirithiwa na mama yake (Mama Ngina)
na ndugu wa familia nzima. Kama kweli Uhuru Kenyatta ataamua
kuwarudishia ardhi wasio na ardhi nadhani itakuwa kama kuwahonga wapiga
kura kwa sasa. Isipokuwa Uhuru Kenyatta kukataa kuwa yeye si mfaidika wa
ukwapuaji ardhi Kenya inatufikisha mahali tuwe makini na wanasiasa wetu
wa kiafrika. Ni waongo sana na si watu wa kukubali ukweli na kuukabili
kama ulivyo.
Kwa upande wa Raila Odinga, yeye amekazia kumshambulia Uhuru Kenyatta na
anawaahidi wakenya wakimchagua atahakikisha wenye ardhi kubwa
wanazirudisha. Sina hakika kama yuko sahihi, ikumbukwe kuwa Kenya sasa
inatawaliwa na Katiba mpya kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita sasa; na
ukiisoma Katiba ya Kenya ndicho chombo pekee ambacho kimeweka utaratibu
wa kuhakikisha wale walionyang’anywa ardhi wanarudishiwa.
Hakuna mwanasiasa yeyote atakayeweza kurudisha au kunyang’anya mtu
ardhi.
Kama Raila Odinga anataka kuwa mkweli, ni bora aeleze ni jinsi gani
atasimamia kuhakikisha Sera ya ardhi, Sheria ya Ardhi na Katiba ambayo
imeweka kipengele (Sura nzima) maalum kueleza ni jinsi gani watu
waliopoteza ardhi watarudishiwa au kulipwa fidia ya ardhi yao. Sera ya
ardhi ya Kenya imeelezea kinagaubaga juu ya historia ya tatizo la ardhi
nchini Kenya na ikaweka njia mbadala kutatua tatizo hili. Hii imejenga
msingi kwa Katiba mpya ya Kenya kutekeleza sera ya ardhi.
Kwa ujumla, kampeni hii ya kufufua chuki za wazazi wa wagombea ni
kielelezo kingine kuonesha kuwa kwa kiasi fulani wanasiasa wetu ni
wabinafsi zaidi na kwenye kampeni hawazungumzi mambo ya msingi (issues)
bali wanabakia wakizungumza siasa katika kutafuta mvuto wa kisiasa zaidi
(political mileage). Tunapojiandaa kwa mabadiliko ya kisiasa Tanzania
tunapaswa kuyachambua kwa kina matamko ya wanasiasa wetu.
No comments:
Post a Comment