MWANANCHI
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro amepiga
marufuku unywaji wa pombe kali aina ya Viroba kwa watu wenye umri kati
ya miaka 18-30 pamoja na kupiga marufuku uuzaji wa pombe kiholela.
Waraka uliotolewa na Mkuu wa Mkoa huyo
umeonyesha kuanzia Desemba 15 Serikali itaendesha oparesheni maalum ya
kuwakamata watu wanaolewa pombe muda wa kazi.
Akielezea hilo Mkuu huyo wa Mkoa amesema
ulevi uliokithiri umepelekea kupungua kwa nguvu kazi ya kutosha
kutokana na vijana wengi kujiingiza katika unywaji wa pombe unaoathiri
afya zao.
MWANANCHI
Mtu mmoja amefariki kutokana na tetenasi
ambayo ilisababishwa na kidonda alichokipata wakati anabandua kucha za
bandia alizobandika wakati siku ya harusi yake.
Mtu huyo Sophia Komba alifunga ndoa
Oktoba 15 na Richard Mmary, ambapo mume wake anasema wiki moja baada ya
kufungwa ndoa hiyo Sophia alimuaga anaenda saluni kutoa kucha,
aliporudi baada ya saa mbili alikuwa analalamika sana kuumwa na kidole
ambacho kilipata kidonda kutokana na kubanduliwa kucha vibaya na kuumia.
Mume wake anasema hakujua ukubwa wa
tatizo hivyo akamnunulia Spirit na kumpaka, lakini tatizo likaendelea
kuwa kubwa na mpaka anafariki daktari alithibitisha kuwa mwanamke huyo
amefariki kwa tetenasi.
Wamiliki wa saluni waliohojiwa wamesema
kuwa gundi inayofaa kubandikia kucha huuzwa ghali hivyo huenda saluni
iliyomhudumia marehemu huyo walitumia gundi ya bei nafuu ambayo siyo
salama, huku mtu mwingine anayejishughulisha na kubandika kucha hizo
akisema iwapo kucha hizo zinakaa muda mrefu huwa na madhara kwa
binadamu.
NIPASHE
Zahanati ya Mtepeche iliyopo Wilayani
Nachingwea, Lindi inakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa mzani wa
kupimia watoto baada ya kuzaliwa kwa zaidi ya kipindi cha mwaka mmoja,
huku uchunguzi wa gazeti hilo ukibaini kuwa mzani mmoja unagharimu kati
ya shilingi 250,000/- na 300,000/-.
Mganga Mfawidhi wa Zahanati hiyo
Ibrahimu Mpini amesema changamoto hiyo imefanya wasijue uzito wa watoto
wanaozaliwa na jitihada walizozifanya hazijazaa matunda yoyote mpaka
sasa Zahanati hiyo kuwa na mzani.
Mbali ya changamoto hiyo, Zahanati hiyo
inakabiliwa pia na tatizo la ukosefu wa glovu na pia upungufu wa dawa
muhimu ikiwemo Panadol.
JAMBO LEO
Rais wa Malawi Profesa Peter Mutharika
ameibuka na kusema kuwa Tanzania haina hata sentimeta moja kwenye Ziwa
Nyasa mbele ya Marais Wastaafu Joachim Chissano wa Msumbiji na Festus
Mogae wa Botswana walipokutana Malawi.
Rais huyo amesema hayo wakati mgogoro wa mpaka kati ya Malawi na Tanzania ukiwa haujapatiwa ufumbuzi.
“Suala hili liko wazi kabisa kwa mujibu
wa Mkataba wa Heligoland wa mwaka 1896 na muafaka wa OAU (sasa Umoja wa
Afrika- AU) wa mwaka 1985” alisema Mutharika.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, Bernard Membe aliwahi kukaririwa akisema nchi zote husika
zinapaswa kuheshimu maagizo ya kuwasilisha ushahidi wa mipaka katika
Sekretarieti ya SADC kwa wakati ili wasuluhishi waupitie.
JAMBO LEO
Mkulima na mkazi wa kijiji cha Rosana
Wilaya ya Tarime, Matiku Makenge Ghati ameuawa na watu wasiojulikana kwa
kukatwa mapanga kichwani.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tarime-Rorya,
Kamishna Msaidizi Benedict Lazaro Mambosasa amethibitisha kutokea kwa
tukio hilo na kusema kuwa marehemu kauawa jirani na nyumba yake akiwa
anatoka matembezini, mpaka sasa hakuna aliyebainika kuhusika na tukio
hilo na upelelezi unaendelea.
Mambosasa alitoa wito kwa jamii kutoa
taarifa pale wanapoona vitendo vya kiarifu vinajitokeza ili Jeshi hilo
lifike mapema na kuwatia nguvuni watuhumiwa wa tukio husika.
HABARI LEO
Mkazi wa Temeke Leonidas Mathias (42)
ambaye ni mwalimu amefikishwa kizimbani katika Mahakama ya Mwanzo
Kariakoo kujibu mashtaka ya kumshambulia Askari wa Usalama Barabarani
Koplo Machage Novemba 10, Barabara ya Uhuru maeneo ya Clock Tower.
Mathias ameshtakiwa kwa kosa la kumkaba
Askari huyo akiwa amevalia sare ya kazi, mshtakiwa amekana kosa hilo na
kurudishwa rumande mpaka Desemba 3 ambapo kesi hiyo itatajwa tena.
HABARI LEO
Ofisa Elimu Taaluma Mkoa wa Rukwa,
Fanuel Mkaruka amesema wanafunzi 808 wa kike kutoka shule za msingi na
Sekondari Rukwa wamekatiza masomo yao baada ya kupata ujauzito katika
kipindi cha miaka minne iliyopita, ambapo kati yao 59 ni wanafunzi wa
shule ya msingi huku 749 wakiwa wa sekondari.
Zimetajwa baadhi ya sababu kubwa
zinazopelekea wanafunzi wengi wa kike kuacha masomo kuwa ni pamoja na
mimba na tatizo la fikra iliyojengeka kwa watu wengi kwamba mtoto wa
kike ni wa kuolewa tu.
Amezitaja baadhi ya changamoto
zinazofanya changamoto hizo kuendelea kuwepo kuwa ni pamoja na wasichana
wanaopewa ujauzito kutotoa ushirikiano kwa vyombo vya dola kuwataja
wahusika.
Ofisa mradi wa unaofadhiliwa na Sweden
TMEP Fausta Valery amesema mradi huo umechangia kupunguza tatizo hilo
kwa asilimia 10 pekee.
UHURU
Victor Kanyari ambaye anayeendesha
kanisa la Salvation Healing Ministry amegundulika kuwa ni tapeli baada
ya kufichuliwa na kipindi cha Tv cha “Inside Story” baada ya kubainika
juu ya mchezo anaoufanya na kundi la wafuasi wake ambao hutoa ushuhuda
wa uongo kwa kujifanya wamepona.
Jamaa huyo ambaye amekuwa akifanya
huduma zake Nairobi Kenya aliweza kujikusanyia imani za watu wengi kwa
kuwa amekuwa akilenga masikini ambao walikuwa tayari kutoa kidogo
walichonacho ili wapate msaada wa mchungaji huyo.
Baada ya jamaa huyo kugundulika
imepelekea Serikali kupiga marufuku usajili wa makanisa mapya, huku
kukiwa na agizo la makanisa yote kujisajili, agizo ambalo limeonekana
kutozingatiwa.
Moja ya watu waliohojiwa amesema; “..
Kanyari ni Mkenya wa kawaida, mwenye njaa, anayetafuta kula, hadhi na
madaraka. Kama mtu aliyekuwa naye darasani hivi sasa ni mbunge na
anaweza kumpita akiendesha gari la kifahari atajiuliza ‘Nimewezaje name kuendesha kama hilo’..”by
No comments:
Post a Comment