Tuesday, March 24, 2015

DMO HAI KATIKA KASHFA

Na Charles Ndagulla,Moshi.
MGANGA  Mkuu wa Hospital ya wilaya ya Hai (DMO) mkoani Kilimanjaro,Paul Chaote,ameingia katika kashfa nzito akituhumiwa  kuwadhalilisha kwa kuwatumikisha katika vitendo vya ngono baadhi ya wauguzi na waganga wa kike wa hospital ya wilaya.
Tuhuma hizo nzito zipo kwenye andiko la kurasa mbili la watumishi wa Idara ya Afya wilayani Hai ambalo wamelisambaza kwenye vyombo vya habari mwishoni mwa wiki wakituhumu uongozi mbovu wa Mganga huyo mkuu wa wilaya.
Watuhumishi hao ambao majina yao tunayahifadhi kwa sasa kwa sababu za kiusalama,wamedai kuwa bosi wao huyo amekuwa tatizo kubwa kwa watumishi wa Afya wilayani humo hali ambayo wamedai imesababisha kudhorota kwa baadhi ya huduma za afya kwa wagonjwa wa nje na wa ndani.
“Sisi wafanyakazi wa afya wilaya ya hai,tunapenda kutoa masikitiko yatu kupitia gazeti lenu kuhusu unyanyasaji wa watumishi wa afya,hali hii ya unyanyasaji  imesababisha madhara makubwa sana kwa baadhi ya wafanyakazi na wengine kupoteza maisha”inasema sehemu ya andiko hilo.
Wamedai kuwa wafanyakazi watano na idara zao zikiwa kwenye mabano ambao ni Valeria Mlay (RCH) Robert Mashayo (Pharmacy) Glorious Mshindavita(Pharmacy),Grace Mushi na Emmanuel  Nsiri wote kutoka idara ya wagonjwa wa nje (OPD),walifariki dunia kwa nyakati tofauti kutokana na kile kilichodaiwa ni  vitisho kutoka kwa DMO huyo baada ya  kujikuta wakipatwa na magonjwa ya shinikozi la damu,sonona na sukari.
Hata hivyo, Mganga mkuu huyo wa wilaya amekanusha tuhuma zote zilizoelekezwa kwake akiita ni majungu yanayosambazwa na watuhumishi ambao hawafuati taratibu za kazi pamoja na maelekezo kutoka ofisi yake.
Akizungumza kwa njia ya simu akiwa Jijini Dar es salaam mwishoni mwa wiki, DMO huyo alisema kuwa ofisi yake inafanya kazi kwa utaratibu na maelekezo kutoka ofisi ya mkurugenzi wa halmshauri ya wilaya ya Hai aliyedai kuwa ndiye anayemsimamia katika utendaji kazi wake.
Alidai kuwa,hajawahi kuhojiwa na chombo chochote juu ya tuhuma kama hizo na kuongeza kuwa anayesambaza tuhuma dhidi yake anachuki binafsi na ni mtumishi ayependa kufanya kazi kwa utaratibu ulioweka na mamlaka husika.
Watumishi hao katika andiko lao wameorodhesha tuhuma 15 dhidi ya bosi wao ikiwamo udhalilishaji wa watumishi wa kike,kuunda makundi,madaktari kutolipwa fedha kwa ajili ya upasuaji na uchunguzi wa maiti(post-mortem allowance) kwa kipindi cha miaka mine hadi sasa.
Tuhuma nyingine ni pamoja na kufanya upendeleo kwa kuwapeleka kwenye ziara za mafunzo wafanyakazi ambao hutoa aslimia kumi ya posho wanayoipata katika semina hizo,tuhuma ambazo pia mganga mkuu huyo wa wilaya ameziita ni uzushi na kuongeza kuwa ziara za mafunzo hutolewa kulingana na mahitaji ya wahusika.

PROF. MUHONGO KUWANIA URAIS 2015

*Wapambe wasema alisurubiwa kwa ajili ya urais
NA GORDON KALULUNGA, MBEYA
WAKATI joto la urais likizidi kupanda ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutokana na hofu ya baadhi ya majina mazito ya wagombea wa nafasi hiyo kuendelea kujitokeza ikiwa ni pamoja na kujinadi kwa siri, Prof. Sospeter Muhongo, naye amejitosa Katika nafasi kinyang’anyiro hicho, imefahamika.
Kwa mkoa wa Mbeya,  tayari baadhi ya wapambe wake wameanza kazi katika wilaya za Momba, Mbeya Vijijini na Mbeya Mjini huku baadhi ya viongozi wa wanafunzi wa vyuo na vyuo vikuu na waliokuwa katika ngome ya kundi la Edward Lowassa, wanaongoza kazi ya kumnadi kwa wananchi Prof. Muhongo.
Viongozi hao baadhi wameelezwa kuwa walikuwa katika kundi la Vijana wa 4U Movement, linalojinasibu kuwa ni marafiki wa Lowassa.
Mmoja wa wasomi ambaye hakutaka jina lake litajwe, alisema kuwa ameamua kuondoka katika kundi la Lowassa kwasababu mbalimbali ikiwemo kundi hilo kuthamini baadhi ya watu huku wengine hasa wanaofanya kazi kubwa badala ya utapeli kutothaminiwa.
“Hivi karibuni unakumbuka kuwa kulikuwa na kongamano la Vijana wa 4U Movement hapa Mbeya, ni kundi ambalo limeamua kujitafutia fedha kwa migongo ya wengine, jambo ambalo mimi lilinisikitisha na nikaamua kuwaambia hata wakubwa lakini tunapuuzwa” alisema kijana huyo.
Alipoulizwa kuhusu yeye pamoja na wenzake kuamua kumnadai Prof. Muhongo wakati hivi karibuni alijiuzuru kutokana na kashfa ya Escrow, alisema kuwa suala lile mwanasheria Mkuu alisema Bungeni kuwa yeye ndiye anastahili kubeba lawama lakini hakusikilizwa baada ya kubaini kuwa Prof. Muhongo hatakuwa anashikika kwenye Urais hivyo wakaamua kumsulubu baadhi hata bila kujua.
Katika moja ya kikao kilichofanyika katika ukumbi wa Nsungwe Hotel juzi mjini Mbalizi wilaya ya Mbeya Vijijini kati ya wapambe wa kiongozi huyo na vijana wa Bodaboda, vijana hao walielezwa kuwa ni vema wakaanza kuwa na mtazamo chanya wa kumsema vema kiongozi mwenye uaminifu, uadilifu, uzalendo na kuona anataka kutupeleka wapi.
Katika kikao cha wasomi wa vyuo vikuu na wanataaluma kilichofanyika jana katika bustani ya City Pub Jijini Mbeya, wasomi hao wamekubaliana kutompoteza kiongozi huyo huku baadhi wakisifia juhudi zake za kuaminiwa na moja ya Vyuo Vikuu bora kabisa nchini China, The China University of Geosciences (Wuhan), ambacho kwa ushawishi wake kimetoa ufadhili wa masomo katika fani ya Mafuta na Gesi (Oil and Gas Studies) kwa ngazi ya Shahada ya Uzamili na Shahada ya Uzamivu.
“Jumla ya nafasi 22 zitatolewa mwaka huu kwa Watanzania watakaokidhi vigezo, ambapo watapata ufadhili wa masomo hayo kwa asilimia 100 ikiwemo chakula, malazi na gharama za masomo (tuition fee)” alisema mmoja wa kiongozi wa wapambe wa kiongozi huyo mkoani Mbeya.
Prof. Muhongo alipopigiwa simu na mwandish wa habari hizi ili kuthibitisha kama atawania nafasi hiyo ya urais mwaka huu, alisema kuwa, anafahamu taratibu za chama chake hivyo hawezi kukubali au kukataa.
“Mimi nafahamu na kuheshimu taratibu za chama, ukifika wakati chama kikiruhusu kusema nitasema kama nitawania ama la, lakini niseme kuwa ni wakati sasa wa kumpata kiongozi anayeaminika na mwenye uwezo wa kujenga uchumi imara unaotoa fursa kwa kila Mtanzania” alisema Prof. Muhongo.
Aidha alisema yeye amebahatika kukaa karibu na Mwalimu Julius Nyerere na alibahatika kuambiwa nini alikuwa anakusudia kuipeleka Tanzania kwa ajili ya Tanzania itakayoendana na wakati na rasilimali za nchi kuwa tunu kamili za watanzania na siyo kuwa laana.

Friday, March 20, 2015

POLISI WAMALIZA MZOZO TUNDUMA

 KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA, AHMED MSANGI AKIZUNGUMZA NA WAANDISHI WA HABARI LEO NJE YA OFISI YAKE.


JESHI la Polisi mkoa wa Mbeya, limefanikiwa kuzima mzozo na vurugu zilizodumu kwa siku tatu eneo la Tunduma wilaya ya Momba.

Vurugu hizo zilitokea baada ya mmoja wa kiongozi wa Mtaa wa Makambini kata ya Sogea kuwadanganya baadhi ya wananchi anaowaongoza kuwa alikuwa ameshinda kesi ya Plot ambayo inamilikiwa na Chama Cha Mapinduzi(CCM), na kuamuru uchimbwe msingi ili ijengwe Hospitali.

Baada ya hali hiyo kujitokeza, baadhi ya viongozi wa CCM walitoa taarifa Polisi ambapo pande mbili ziliitwa na kusikilizwa ambapo kesho yake Machi 15, mwaka huu, kiongozi wa Chadema akawa ameenda tena na wafuasi wake kwa ajili ya kuchimba msingi wa Hospitali hiyo ambayo walihitaji kuijenga bila hata kuwa na ramani na pia kutofahamu kuwa Hospitali haijengwi ngazi ya Mtaa na hata umilikaji wa ardhi haupo kisheria ngazi ya Mtaa bali kitongoji.

Akizungumza na waandishi wa habari leo mkoani Mbeya, Kamanda wa Polisi Ahmed Msangi, amesema kuwa walipofika Polisi kuwasimamisha wasiendelee na zoezi hiyo, wakaanza kurusha mawe na walipojaribu kutawanywa, wakaanza kuchoma matairi katikati ya barabara na kuzua tafrani zaidi.

Alipoulizwa kuwa kuna nguvu kubwa ilitumika katika kudhibiti ghasia hizo, alisema kuwa nguvu iliyotumika ni ya kawaida na ilitumika kutokana na tukio lenyewe lilivyokuwa na kufanikisha kurejesha amani na kwamba isingetumika nguvu ambayo imetumika isingewezekana kuzima ghasia hizo ambazo alidai kuwa zilikuwa zikifanywa na wahuni pamoja na baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa.

MWAKABWANGA AWAMWAGIA MILIONI MBILI WAENDESHA PIKIPIKI MBARALI





 Mwenyekiti wa chama cha waendesha bodaboda mji wa Rujewa wilayani Mbarali mkoani Mbeya, Shabani Tambalamandu, akizungumza neno. Kulia ni ndugu Mwakabwanga katika ukumbi wa Polisi mjini Rujewa.

 


MWENDESHA pikipiki maarufu nchini, ambaye pia ni mfanyabiashara katika sekta ya usafirishaji na kamanda wa UVCCM wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya, Ibrahim Ismail (Mwakabwanga), amewapatia kiasi cha Shilingi Milioni mbili, waendesha bodaboda wa Rujewa wilayani hapa kwa ajili ya kukopeshana.

Tukio hilo lilifanyika katika ukumbi wa mikutano wa Jeshi la Polisi wilaya ya Mbarali juzi, ambapo pamoja na kukabidhi fedha hizo, alisema kuwa anatarajia kufanya mazungumzo na wataalam wa kutengeneza pikipiki nchini China, kisha kupeleka wilayani humo na kufungua duka ambalo waendesha pikipiki hao watanunua kwa bei nafuu na asilimia fulani itakuwa inaingia katika mfuko wao.

“Ujasiliamali huu ulianzishwa na kuhamasishwa nchini na kiongozi mmoja ambaye leo hii simtaji jina lake, lakini ukifika wakati nitamtaja. Nafurahi kuona umoja wenu wa waendesha pikipiki hapa Rujewa na kuanzia leo nawapa jina la wapiga raba au wachapa mwendo, badala ya kuitwa bodaboda maana hapa hatuendi mipakani” alisema Mwakabwanga.

Alisema kuwa yeye ni dereva kwa miaka 38 na mwendeshaji wa pikipiki kubwa na kwamba usafirishaji unaofanywa na vijana hao ni muhimu kuheshimiwa kwasababu ndiyo usafiri pekee unaoweza kumfikisha abiria sehemu anayohtaji kwa wakati anaoutaka.

“Madhara makubwa ya ajali za pikipiki yapo kwenye mwili wa binadamu na wala siyo barabara, chapeni mwendo kwa nidhamu na mjiepushe kutumika kuharibu taifa letu na mtambue kuwa vijana maisha yenu ni tunu na msiombee kumaliza matatizo yenu siku moja maana ukimaliza matatizo unatakiwa ufe” alisema huku akishangiliwa na vijana hao wakisindikizwa na wimbo unaoitwa Bodaboda.
Awali akisoma risala fupi mbele ya ugeni huo, Katibu Mkuu wa chama hicho cha wachapa raba Rujewa, Amos Kihodogo, alisema chama chao kilianzishwa mwaka 2010 na wanachama 18 ambapo kwa sasa kina wanachama 130 na wanachangishana Shilingi 2,000/= kila mwezi kwa ajili ya kuimarisha mfuko wao na kukopeshana.

“Kila mwezi tunakusanya Tsh. 260,000/=, fedha ambazo zinatusaidia kwenye matatizo hususani misiba, ugonjwa, sherehe pamoja na tatizo la kuibiwa pikipiki kwa wanachama” alisema Kihodogo.

Alieleza kuwa, kutokana na mipango yao, wanahitaji kuwa na kiasi cha Shilingi Milioni 10, lakini kwa sasa wanayo akiba ya shilingi Milioni mbili tu.

Mwenyekiti wa chama hicho, Shabani Tambalamandu, alisema kuwa pamoja na uhitaji wa shilingi milioni nane, wanahitaji udhamini wa kukopeshwa pikipiki kwasababu wengi wao wanaendesha pikipiki ambazi siyo mali zao.

Akijibu ombi hilo, mbali na kutoa Shilingi Milioni mbili, alisema kuwa matatizo mengine yanaweza kuishia Dodoma ambako aliwaomba wamteue mmoja wao aambatane na msafara wa pikipiki unaotarajia kuanza safari kesho Jumamosi kutoka Mbarali kuelekea mjini Dodoma ambako kuna kiongozi ataupokea.

POLISI; WANANANCHI WANAFICHA WAHALIFU. WAGANGA WAKAMATWA NA NYARA ZA SERIKALI

Kamanda wa polisi mkoa wa Mbeya, Ahmed Msangi.

 Baadhi ya ngozi za wanyama ambao ni nyara za serikali, zikiwa chini ya ulinzi mkali wa askari Polisi mkoani Mbeya, zinazosemekana zimekamatwa katika oparesheni ya kusaka waganga wa kienyeji wapiga ramli chonganishi.
 Kamanda wa polisi mkoa wa Mbeya, Ahmed Msangi, akiwaonesha waandishi wa habari mkoani humo leo kucha za Chui na mbwa mdogo aliyekaushwa, vitu ambavyo amesema zimekamatwa kwa waganga wa kienyeji wapiga ramli chonganishi.

  Kamanda wa polisi mkoa wa Mbeya, Ahmed Msangi akionesha kucha za Chui.
  Kamanda wa polisi mkoa wa Mbeya, Ahmed Msangi, akionesha baadhi ya vitu na tunguli zilizokamatwa kwa waganga wa jadi wapiga ramli chonganishi.


  Kamanda wa polisi mkoa wa Mbeya, Ahmed Msangi, akionesha baadhi ya vitu na tunguli zilizokamatwa kwa waganga wa jadi wapiga ramli chonganishi.
JESHI la Polisi mkoani Mbeya, limesema kuwa moja ya changamoto inayowakabili katika utendaji kazi zao, ni pamoja na baadhi ya wananchi kuwaficha wahalifu wakiwemo Waganga wa kienyeji wanaopiga ramli chonganishi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ahmed Msangi, ameyasema hayo leo ofisini kwake, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari na kutoa taarifa kuhusu msako unaoendelea wa kuwasaka na kuwakamata waganga wanaopiga ramli chonganishi mkoani hapa.

Amesema katika oparesheni hiyo iliyoanza mwanzoni mwa mwezi huu, imefanikisha kukamatwa watuhumiwa 23 ambao baadhi yao wamefikishwa mahakamani na wengine wanaendelea kuhojia.

Alivitaja baadhi ya vitu ambavyo wamekutwa navyo baadhi ya waganga hao kuwa ni pamoja na zana/vitendea kazi zikiwemo nyara za serikali.

Baadhi ya nyara za serikali alizozitaja na kuzionesha mbele ya maafisa wa Jeshi hilo na baadhi ya waandishi wa habari kuwa ni Konokono 2 wa baharini, Mafuta ya Simba, Mifupa ya kakakuona, Vipande vitatu vya ngozi ya Chui, kucha za Chui, Mkia wa farasi, mifupa ya wanyama aina mbalimbali wa porini, kipande cha Nungunungu, mikia mitano ya paka pori na Pembe tatu za mnyama digidigi.

Nyara zingine ni mguu mmoja wa Nyani, mguu mmoja wa ndege aina ya Tai, mguu mmoja wa mnyama aina ya Nyegere, Pembe nne za swala na Ngozi ya Mamba.

Zana ambazo siyo nyara za serikali walivyokamatwa navyo alisema na kuvionesha kuwa ni Usinga, Biblia mbili za kabila la / Lugha ya Kinyasa, Mbwa mdogo aliyekaushwa kwa moshi, vitambaa. vioo, vibuyu vidogo vyenye shanga vikiwa na vitu vidhaniwavyo kuwa ni dawa asilia za aina mbalimbali, Fimbo nyeusi, msalaba na Pembe za Ng'ombe.

Kamanda Msangi ametoa wito kwa jamii kujiepusha na tabia ya kusadiki imani potofu za kishirikina kwa kupiga ramli chonganishi kwa nia ya kutaka kutatua matatizo yao kwani hali hiyo inahatarisha usalama, umoja na mshikamano miongozi mwa jamii na kuleta chuki na uhasama, badala yake wamche Mungu.

Aidha ameomba wananchi wenye taarifa za walipo waganga na wahalifu wengine kutoa taarifa kwa mamlaka husika ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.

No comments:

Post a Comment