CHAMA kipya cha Kutetea Haki na Maslahi ya Walimu Tanzania (CHAKAMWATA)
kimesajiliwa rasmi na kupata cheti cha usajili wa kudumu kutoka Wizara
ya Kazi na Ajira.
Akizungumza na
FikraPevu,
Katibu Mkuu wa Chakamwata, Mwalimu Meshack Kapange, anasema chama hicho
kipya kinaundwa na walimu nchini waliojiondoa kutoka mikononi mwa Chama
Cha Walimu Tanzania (CWT). Kapange amesema mchakato wake wa kukisajili
chama hicho ulianza miaka minne iliyopita, hadi hivi juzi kilipopewa
usajili wa kuendelea na shuhuli zake kisheria.
“Ni furaha iliyoje kupata usajili huu wa chama chetu cha kutetea haki
na maslahi ya walimu? Huu ni ukombozi kwa walimu wanaokatwa asilimia
mbili za mishahara yao bila kurejeshewa wanapostaafu,” anasema Katibu
Mkuu huyo.
Kuundwa kwa chama kipya hicho kumetajwa na wachambuzi wa mambo kwamba
kunaweza kuipasua CWT na pia kutahitimisha ukiritimba wa muda mrefu
mrefu wa chama hicho. Aidha, chama hicho kitatoa fursa sasa kwa walimu
nchini kuwa na hiyari ya kujiunga na chama ambacho wataona kina maslahi
kwao badala ya ilivyo sasa ambapo walimu walikuwa hawana chaguo zaidi ya
kujiunga na CWT.
Kwa mujibu wa Mwalimu Kapange, Makao Makuu ya sasa ya chama hicho
yatakuwa Jijini Mbeya.
Anasema walimu watakaohitaji kujiunga na chama
hicho kipya, watafanya hivyo kwa hiari yao kama sheria za kazi
zinavyoelekeza tofauti na CWT ambayo kila mwalimu anayepata ajira
serikalini alikuwa analazimishwa kujiunga na kuanza kukatwa fedha zake
kutoka kwenye mshahara wake bila ridhaa yake na kinyume cha sheria za
ajira.
“Kila mwanachama atachangia asilimia moja tu ya mshahara wake kwa kila
mwezi badala ya asilimia mbili kama ilivyo kwa CWT. Wakati mwanachama
anapostaafu, atapewa ‘bonus’ kama asante kwa kuchangia Chama,” anasema
Mwalimu Kapange.
Mbali na hilo, Kapange anasema Chakamwata kitafanya jitihada za
kuwajengea wanachama wake uwezo wa kutambua wajibu wao, haki zao na
jinsi ya kuzidai, badala ya kutambua wajibu pekee kama ilivyo ndani ya
CWT, kwa maelezo kwamba hakuna wajibu kwa mtumishi yeyote wa umma
usiokwenda sambamba na haki yake.
“Tulipokuwa tukiomba usajili kwa mara ya kwanza Mei, 2012, tulikuwa
wanachama 400 ingawa masharti ya kisheria ya kuanzisha vyama kama hivi
yanataka wanachama 20 tu. Nashukuru kwamba hadi tunapata usajili huu,
wanachama wetu wanafikia 9,743, wengi wao wakitokea mikoa ya Mbeya,
Iringa, Njombe, Rukwa, Ruvuma, Arusha, Mara, Morogoro, Singida na
Kagera,” amesema.
Chama kipya hicho, kabla hakijasajiliwa, kilikuwa kikijulikana kwa jina
la Umoja wa Maofisa Elimu Tanzania (UMET). Hata hivyo, uongozi wa muda
wa chama hicho ulikaa tena na kukipa chama hicho jina la
Chakamwata. Chama hicho kimepewa usajili kwa namba 031, huku cheti chake
kikiwa kimesainiwa na Msajili wa Vyama Huru vya Wafanyakazi na Waajiri
nchini, Doroth Uiso.
FikraPevu
inaendelea kumtafuta Rais wa CWT, Gratian Mukoba, pamoja na maoni ya
walimu mbalimbali nchini, ili pamoja na mambo mengine, waweze kuelezea
ujio wa chama kipya hicho cha walimu nchini na athari zake katika
mstakabali wa mshikamano na utengamano wa walimu nchini katika siku za
usoni.