VITA YA KUGOMBEA URAIS 2015 WASHIKA KASI MTANDAONI...FACEBOOK,TWEETER NA WHATSAPP ZITTO KABWE MAKAMBA TEAM LOWASSA ZAONGOZA

Ikulu ya Tanzania
Wakati
safari ya kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu ikipamba
moto, kumeibuka makundi ya watu yaliyofungia akaunti katika mitandao ya
kijamii yakiwaunga mkono baadhi ya wanasiasa waliotangaza au wanaotajwa
kuwa na nia ya kugombea urais ya kuwashambulia washindani wao.Kila
kundi limejipatia wafuasi wengi ambao wanaonyesha kumkubali mwanasiasa
husika wanayedhani anafaa kuwa rais wa Tanzania endapo atapitishwa na
chama chake na kupigiwa kura na wananchi.Hata
hivyo, wasomi na wachambuzi wanaonya kuwa pamoja na njia hii kuwa ya
haraka kuwafikia wapigakura walio wengi ambao ni vijana na wanawake,
inatakiwa kutumika kwa uangalifu la sivyo inaweza kusababisha machafuko.
Makundi yenyewe
Makundi
hayo, mengi yakipatikana katika mitandao ya Facebook, Twitter na
WhatsApp yanafanya kazi ya kuwanadi wanasiasa na kubainisha shughuli
mbalimbali wanazozifanya kila siku wawapo katika ziara zao za binafsi,
za kiserikali au kichama katika maeneo mbalimbali nchini.
Baadhi
ya kurasa za makundi hayo zenye wafuasi wengi ni pamoja na ule wa ‘Team
Lowassa’, kundi linalomuunga mkono Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa
ambao hadi jana ulikuwa na wafuasi 46,124 ambao wanaweza kupata habari
mbalimbali zinazomhusu kiongozi huyo.
Hata
hivyo, mbunge huyo ambaye pia aliwahi kuwa waziri mkuu, hivi karibuni
alikaririwa na gazeti hili akiikana moja ya akaunti za Twitter iliyokuwa
imechapisha taarifa zilizomkariri akizungumzia suala la ufisadi wa
escrow.
Akizungumzia
kurasa hizo, Msaidizi wa Lowassa, Abubakar Liongo alisema akaunti hizo
zinatengenezwa na marafiki na kusisitiza kwamba kiongozi huyo hahusiki
nazo kwa namna yoyote.
“Hawa
ni marafiki tu, huwezi kuwazuia kufanya wanachotaka kufanya, sisi
tumeshatoa taarifa kuwa hizi hatuhusiki nazo,” alisema Liongo.
Kundi
jingine linajitambulisha kama ‘Team Hamis Kigwangalla’ linalomuunga
mkono Mbunge wa Nzega, Dk Hamis Kigwangalla na mpaka kufikia jana
lilikuwa na wafuasi 9,893. Hili ni kundi la pili kuwa na wafuasi wengi
katika mtandao wa Facebook baada ya lile la Team Lowassa.
Ukurasa
mwingine umeanzishwa na watu wanaomuunga mkono Mbunge wa Bumbuli na
Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba.
Ukurasa huu umepewa jina ‘January Makamba – The next President’ na hadi
jana ulikuwa na wafuasi 7,075.
Wanasiasa
wengine wanaohusishwa na mitandao hiyo ni Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe ambaye mbali na akaunti yake
kwenye WhatsApp, ukurasa wa marafiki zake kwenye Facebook wenye jina la
‘Bernard Membe Fans Page’ umefikisha wafuasi 5,120.
Kundi
la wafuasi wa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbrod Slaa linafuatia.
Kundi hilo lililoanzisha mtandao uliopewa jina ‘Dr Slaa Team Winner –
2013/2015’ hadi jana lilikuwa na wafuasi 4,337.
Vilevile,
lipo kundi jingine linalomuunga mkono Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais
(Uhusiano na Uratibu), Stephen Wasira na ambalo ukurasa wake uitwao
‘Wasira wa Watanzania (WWW)’ lina wafuasi 3,524.
Pia
upo ukurasa wa “Marafiki wa Samwel Sitta’ katika Facebook wenye
mashabiki 2,238 wanaomuunga mkono Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta.
Katika
mtandao wa Twitter, wanasiasa hao na wengine hawako nyuma, karibu kila
mmoja ana akaunti binafsi huku wafuasi wao wakipata nafasi ya kusoma
yale wanayoyaandika wakati wowote.
Miongoni
mwa wanasiasa wenye wafuasi wengi ni Zitto Kabwe ambaye watu 208,294
wanafuatilia hoja zake na wakati mwingine kujibizana.
Anayefuata
ni Makamba mwenye wafuasi 151,822, Bernard Membe (45,889) na Dk Slaa
(40,830). Lazaro Nyalandu aliyetangaza wiki iliyopita kuingia katika
mbio za kusaka urais, akaunti yake ya Twitter inafuatiliwa na watu
36,726.
Wengine
katika mkondo huo ni Dk Khamis Kigwangalla (26,322), William Ngeleja
(11,110), Anna Tibaijuka (8,053), Freeman Mbowe (4,162), Asha-rose
Migiro (4,736), Edward Lowassa (2,123), Stephen Wasira (750) na Dk
Emmanuel Nchimbi (515).
Ni
dhahiri kuwa wanasiasa vijana ndiyo wanaotumia zaidi mitandao ya
kijamii na kuwa na wafuasi wengi ambao wengi wao pia ni vijana.
Maoni ya wachambuzi
Baadhi
ya wasomi nchini wameelezea kuwa si jambo baya kutumia mitandao ya
kijamii kujinadi kwa wananchi. Hata hivyo, wameonyesha wasiwasi kwa
jinsi inavyotumika na kuwa inaweza kusababisha machafuko.
Mhadhiri
wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Hamad Salim alisema kadri muda
unavyokwenda, ndivyo jamii inavyobadilika na mabadiliko haya yanahusisha
pia matumizi ya mitandao ya kijamii.
Salim
alisema vijana na wanawake ambao ndiyo idadi kubwa ya wapiga kura, sasa
wanatumia mitandao ya kijamii. Alisisitiza kuwa hii ndiyo sababu pekee
iliyowasukuma wanasiasa kuanza kutumia mitandao ya kijamii.
“Mitandao
hii inawasaidia wanasiasa kujitangaza kwa wananchi, pia haina gharama
kwao. Tulizoea kuona wanasiasa wakipita mitaani kutoa zawadi na kujinadi
kwa wananchi kipindi cha uchaguzi, sasa ni rahisi,” alisema.
Hata
hivyo, Salim alionya kuwa mitandao ya kijamii isipodhibitiwa
kikamilifu, inaweza kusababisha machafuko ya kisiasa kama ilivyotokea
katika nchi za Tunisia na Libya na kusababisha mapigano ya wenyewe kwa
wenyewe ambayo yanaendelea mpaka sasa.
“Tuliona
pia wakati wa sakata la escrow, watu walianza kuunda baraza la mawaziri
mtandaoni kabla hata Rais hajasema chochote. Sasa hii ni hatari, wakati
mwingine inaweza kujenga chuki,” alisema.
Alisema
katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika hivi karibuni, Ukawa
hawakutumia nguvu kubwa kwa sababu walishajenga ngome kwenye mitandao ya
kijamii.
Mhadhiri
wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Richard Mbunda alisema sasa
hivi mitandao ya kijamii ni sehemu ya maisha ya Watanzania. Hivyo,
inakuwa rahisi kwa wanasiasa kuwafikia wengi ndani ya muda mfupi kwa
njia hiyo.
Alisema
uzuri wa mitandao ya kijamii ni kuwa wanasiasa wanapata nafasi ya
kujitangaza na wananchi pia wanapata kuwafahamu na kuwapima kama
wanaweza kuongoza Taifa hili.
Aliuangana
na Salim akisema kuwa Tanzania haina udhibiti mzuri wa mitandao ya
kijamii, jambo linaloweza kusababisha chuki na mifarakano miongoni mwa
wanajamii.
“Si
kila linaloanzishwa ni jema asilimia 100, wengine wanatumia mitandao ya
kijamii kuwachafua wengine, hasa mahasimu wao kisiasa,” alisema Mbunda
na kuitaka Serikali kuwa na udhibiti wa mitandao hiyo hasa wakati huu
kuelekea Uchaguzi Mkuu.
chanzo: gazeti la mwananch
No comments:
Post a Comment