Kuasi kwa afisa mwandamizi wa al-Shabaab kwachochea mjadala juu ya programu ya msamaha
Kuasi kwa mkuu wa zamani wa intelijensia wa al-Shabaab, Zakariya Ismail
Ahmed Hersi, kumechochea mjadala juu ya mpango wa msamaha wa serikali ya
Somalia na faida za kuwasamehe maafisa wa al-Shabaab wanaotaka
kujiondoa kwenye kundi hilo.
Vikosi vya usalama vikiwapekuwa wananchi
wakati wa operesheni dhidi ya al-Shabaab mjini Mogadishu tarehe 8
Disemba 2014. Al-Shabaab imekuwa ikilaumiwa kuhusika na mauaji kadhaa
yaliyowalenga wanasiasa, raia waliorejea nyumbani na yeyote mwenye
mahusiano na kampuni za kigeni au serikali. [Mohamed Abdiwahab/AFP]
Hersi, aliyejisalimisha kwa wanajeshi wa Somalia walioko kwenye mkoa wa
Gedo tarehe 27 Disemba, alikuwa anatakiwa na serikali ya Marekani kwa
dau la dola milioni 3. Aliiasi al-Shabaab akiwa na watu wake wachache
siku kadhaa baada ya muda wa msamaha uliongezwa na Rais Hassan Sheikh
Mohamud kukaribia kukamilika.
"Ninaweza kuthibitisha kwamba siku chache zilizopita Zakariya Ismail
Ahmed Hersi alikuja kwenye mikono ya serikali [ya shirikisho] na sasa
anashikiliwa na vyombo vya usalama mjini Mogadishu," msemaji wa
serikali, Ridwan Haji Abdiweli aliiambia Sabahi siku ya Ijumaa (tarehe 2
Januari).
Abdiweli alisema hakujua ikiwa msamaha wa rais utaendelea kwa mwaka huu,
lakini akasema tangazo juu ya suala hilo litatolewa baadaye.
Kujisalimisha kwa Hersi kunaipa serikali ya Somalia fursa ya kuongeza
uwezo wake wa kujua kazi za ndani za kundi hilo la wanamgambo na
kuwasaka wengine wanaotaka kujiondoa kwenye kundi hilo, wanasema
wachunguzi wa masuala ya usalama.
Vile vile kunatoa fursa kwa serikali kujitathmini upya juu ya namna
inavyowashughulikia wale walioachana na al-Shabaab, alisema kanali
mstaafu wa jeshi, Ahmed Omar Ga'al, ambaye alihudumu kama naibu mkuu wa
usalama wa taifa mkoani Gedo wakati wa utawala wa Mohamed Siad Barre.
Hersi aliondoka al-Shabaab miezi kadhaa iliyopita baada ya kugombana na
kiongozi wa wakati huo wa al-Shabaab, Ahmed Abdi Godane, ambaye aliuawa
kwenye mashambulizi ya anga yaliyofanywa na Marekani mwezi Septemba,
lakini hakuweza kupata fursa ya kuja upande wa serikali, alisema Ga'al.
"Niliambiwa na jamaa zake kwamba mtu huyu alitaka kujisalimisha kabla,
lakini alikuwa akiogopa kwa kuwa hakuwa akiiamini programu ya msamaha ya
serikali," alisema.
Wakati rais alipotangaza kwamba serikali ingeliongeza muda wa msamaha
kwa wale wanaojiengua na al-Shabaab, kungelikuwa na mpango wa
kujipenyeza kwenye kundi hilo kama njia ya kukusanya taarifa za
kiintelijensia na kuwapa wapiganaji taarifa juu ya namna ya kuondoka,
alisema Ga'al.
Vyombo vya usalama vya Somalia vilipaswa kujua juu ya ugomvi wa Hersi na
Godane na kumfikia kumpa nafasi ya kupatiwa msamaha, alisema.
Kuifanya programu hii ya msamaha kufanya kazi vyema huko mbeleni, serikali inapaswa kuwa na mikakati mitatu, alisema.
"Kwanza, itumie pesa kuwavutia watu wengi kujiondoa al-Shabaab. Pili,
itumie fursa panapotokezea migogoro ya ndani ya kundi la adui na
[wanachama] wanaotaka kujajusiana. Tatu, watu wenye uzalendo lazima
wawekwe ndani ya adui ili waweze kuiokoa nchi."
Ga'al alisema kufuata hatua hizo kutarahisisha upatikanaji wa taarifa za
kiintelijensia zenye maana na kuishinda al-Shabaab. "Ni kwa kuwa na
taarifa ndipo unapokuwa na uwezo dhidi ya adui yako," alisema.
Mafunzo kutoka waliojisalimisha awali
Profesa Yahye Ali Ibrahim, rais wa Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Somalia,
alisema serikali ya Somalia inapaswa kutekeleza ahadi yake ya kuwapokea
wanamgambo walioasi al-Shabaab kwa mikono wazi.
"Vile ambavyo serikali inamtendea Zakariya na watu kama yeye kutaamua
ikiwa viongozi wengine zaidi wa al-Shabaab na wapiganaji wao
watajisalimisha au la," Ibrahim aliiambia Sabahi, akiongeza kwamba ikiwa
viongozi wa al-Shabaab wanaojisalimisha serikalini wanatendewa vyema,
mamia ya wapiganaji waliovunjwa moyo na kundi hilo watashajiishwa
kufuata.
Kujisalimisha kwa kiongozi wa zamani wa al-Shabaab mkoani Puntland,
Sheikh Mohamed Said "Atom" , mwezi Juni na kiongozi wa zamani wa Hizbul
Islam, Sheikh Hassan Dahir Aweys, mwaka mmoja kabla ya hapo ni mifano
ambayo lazima ifanywe kuwa kigezo, alisema.
"Kwa kadiri tulivyoona, Sheikh Atom na Hassan Dahir Aweys wamekuwa
wakitendewa vyema na tunatarajia kwamba Zakariya atatendewa hivyo
hivyo," alisema Ibrahim.
Ibrahim aliitolea wito serikali ya Somalia kuongeza muda wa msamaha ili
kuwekeza kwenye kipindi hiki cha mitihani ambacho al-Shabaab inakipitia.
"Serikali inapaswa kuzingatia watu ambao wamejipanga [kuasi] na kuwapa
muda zaidi," alisema. "Itakuwa vigumu kwa mtu kuondoka ndani ya kipindi
cha mwezi mmoja au miwili kwa sababu kuna njia nyingi ambazo mtu
anapaswa kuzipitia hadi mtu kuweza kuliacha kundi hilo."
Ibrahim pia aliitolea wito serikali ya Somalia kutumia viongozi wa koo
kutafuta kuzungumza na watu wa koo zao ambao ni sehemu ya al-Shabaab na
ambao wanataka kuliacha kundi hilo.
"Kwa mfano, Zakariya alisalimishakatika mkoa ambao ametoka ingawa
angeweza kujisalimisha katika mkoa mwingine. Hii inaonyesha kwamba
alikuwa na imani katika ukoo wake," alisema.
"Hata hivyo, serikali inapaswa kuwa mwangalifu kuhusu wale ambao wana
nyuso mbili [kama mawakala upande huu na upande mwengine], wale ambao
hujifanya wamejisalimisha wakiwa bado wanafanya kazi na al-Shabaab,"
profesa Ibrahim aliongeza. "Suala hilo lazima lifuatiliwe kwa makini."
Hakuna wasiwasi kwamba Hersi angepewa msamaha wa rais katika mtindo ule
ule aliopewa Aweys na Atom kabla yake, alisema Ibrahim Berow Ibrahim,
mwenye umri wa miaka 32, mkazi wa Mogadishu.
"Mtu huyu ni kama wao. Msamaha ulitolewa kwa mwanachama wowote walioasi
kutoka kwa al-Shabaab na kujitokeza mbele kutumia fursa hiyo," Ibrahim
alisema.
Yeye alitetea msamaha wa serikali ilioutoa kwa walioasi al-Shabaab,
akisema hakuna tofauti na wababe wa vita waliofanya uhalifu mkubwa
wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe na sasa wameweka chini silaha zao
na hata kutumikia katika shirikisho na tawala za kikanda.
"Kwa zaidi ya miaka 20 Somalia ilikuwa katika vita, watu wengi
walishiriki katika vita vile. Kama wababe wale wa vita wanashitakiwa,
kwa hivyo Hersi na wengine kama yeye lazima washitakiwe pia," alisema,
na kuongeza kwamba msamaha lazima kuheshimiwa ili nchi iweze kusonga
mbele.
Haki haikwepeki
Lakini Badrudin Ahmed Egale, mwenye umri wa miaka 28 na mkazi wa
Mogadishu, yeye ana mtazamo wa chini wa kusamehe. Alisema hakukuwa na
sababu ya msamaha kwa viongozi wa al-Shabaab ambao wamesababisha
uharibifu usiokadirika katika Somalia na Afrika Mashariki yote.
"Vipi inawezekana kumsamahe mtu ambaye aliua watu wote wale bila sababu?
Je hilo halitasababisha mtu mwingine kufanya kitu fulani kesho na
kusamahewa?" aliiambia Sabahi. "Watu hawa wanapaswa kuadhibiwa ili iwe
hakuna mtu mwingine anayejaribu kuidhuru jamii hii."
Egale alisema kuwa kila mwananchi ni sawa mbele ya sheria na mtu yeyote
anayetenda uhalifu lazima apelekwe mbele ya sheria na kupata adhabu
anayostahiki.
"Mtu huyu hakutenda uhalifu dhidi ya rais au waziri, yeye aliwadhuru na
kuwaua watoto wa baba na mama, yeye alifanya watoto mayatima na
akawafanya wajane wanawake vijana ambao walikuwa ndio kwanza wanaanza
maisha yao," Egale alisema. "Jinsi gani rais anaweza kumsamehe mtu kama
huyo?"
"Zakariya kwa sasa anashikilia nafasi ya mkuu wa upelelezi au Amniyat,
ambacho ni kitengo kikubwa zaidi cha al-Shabaab na ambacho kimeua watu
wasio na hatia," alisema. Ninasema haki haiepukiki na Zakariya na
wengine kama yeye lazima wapambane nayo."
No comments:
Post a Comment