Tuesday, April 21, 2015

WASHINDI WA SAFARI LAGER WEZESHWA KANDA YA MBEYA WATEMBELEA KIWANDA CHA BIA, WAKABIDHIWA VYETI VYA MAFUNZO YA UJASILIAMALI‏

KAMPUNI ya bia Tanzania (TBL) imetenga zaidi ya shilingi Milion 220 kwa ajili ya kuwawezesha wajasiliamali wadogo wadogo ili kuinua mitaji yao ya biashara katika shindano la Safari lager wezeshwa.
Hayo yalibainishwa na Meneja wa Wilaya ya Mbeya wa TBL, Vivianus Lwezaura, alipokuwa akifunga mafunzo ya washindi wa Safari lager wezeshwa awamu ya nne 2014/2015 yaliyofanyika mwishoni mwa wiki katika Hoteli ya Peter Safari iliyopo Ilomba Jijini Mbeya.
Lwezaura alisema kampuni hiyo imekuwa na utaratibu wa kutenga sehemu ya faida yake kwa ajili ya kuwainua wafanyabiashara wadogo kwa kuwapa mitaji kupitia shindano la Safari lager wezeshwa.
Akizungumza na washiriki wa mafunzo hayo, meneja huyo aliwataka washindi wa Safari lager wezeshwa kuwa mabalozi wa kampuni ya TBL waendako ili kuwahamasisha wajasiliamali wengine kujitokeza katika shindano hilo klwa kuwa ni mkombozi wa mtanzania mwenye kipato cha chini.
Alisema shindano linakuwa halina maana kama kampuni inatumia gharama kubwa kutangaza lakini wafanyabiashara wanaojitokeza wanakuwa wachache hivyo kuigharimu kampuni ambayo inatumia fedha nyingi kuwataarifu washiriki kupitia matangazo mbali mbali.
Awali akimkaribisha Meneja huyo ambaye alikuwa mgeni rasmi, Mkufunzi wa Mafunzo hayo  Deodati Bernard, kutoka kampuni ya Huduma ya maendeleo ya biashara(TAPBDS), alisema mchakato wa kuwapata washindi ni mgumu na hakuna upendeleo wowote unaofanyika.
Alisema katika shindano la awamu hii jumla ya Wafanyabiashara 3500 walijitokeza Nchi nzima ambapo Kanda ya Nyanda za juu kusini walikua zaidi ya 1000 lakini baada ya kupitia vigezo na masharti wakachujwa na kubaki 29 ambao walitembelewa bila wao kujijua na hatimaye kupatikana 12.
Aliongeza kuwa hao 12 baada ya kufuzu hatua zote wamepatiwa mafunzo namna ya kuendesha biashara zao kwa faida kabla ya kukabidhiwa vifaa walivyoomba kutoka katika shindano la Safari lager Wezeshwa.
Kwa upande wao washiriki walisema watakuwa mabalozi wazuri kwa wananchi ili kuwahamasisha na wao kushiriki katika mashindano yajayo ambapo washiriki hao walipata fursa pia ya kutembelea kiwanda cha bia cha TBL Mbeya kujionea shughuli zinazofanywa.
 Meneja wa Wilaya(District Manager)wa TBL Mbeya, Vivianus Lwezaura akizungumza wakati akifunga mafunzo ya Washindi wa safari lager wezeshwa kanda ya Mbeya.
 Meneja wa Wilaya(District Manager)wa TBL Mbeya, Vivianus Lwezaura akizungumza na washiriki wakati akifunga mafunzo ya Washindi wa safari lager wezeshwa kanda ya Mbeya.
 Mkufunzi wa washiriki wa safari lager wezeshwa, Deodati Bernard akimkaribisha mgeni rasmi kufunga mafunzo ya safari lager wezeshwa.
 Mkufunzi mwezeshaji, Sizya Puya, akizungumza jambo katika hafla ya kufunga mafunzo ya washindi wa safari lager wezeshwa.
 Meneja wa Wilaya(District Manager)wa TBL Mbeya, Vivianus Lwezaura akikabidhi vyeti kwa washiriki wa safari lager wezeshwa kanda ya Mbeya.

SERIKALI YAANZA KUTATUA MIGOGORO KWA WANANCHI DHIDI YA HIFADHI ZA TAIFA.

 Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu  akiongea na waandishi wa habari.
Mkutano na waandishi wa Habari Ukiendelea

SERIKALI imeazimia kumaliza migogoro yote ambayo ipo kwa wananchi ambapo Wizara ya maliasili na utalii imeanza kuihesabu ili itatuliwe mapema iwezekanavyo ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Chama cha mapinduzi(CCM).
 
Hayo yalibainishwa na, Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari baada ya kumaliza ziara yake wilayani Mbarali, ambapo alisema Serikali imeona ianze upya kufuatilia suala hilo ikiwa ni pamoja na kutatua mgogoro uliopo.
 
Waziri Nyalandu alilazimika kufanya ziara Wilayani Mbarali kufuatia kuwepo kwa mgogoro wa wananchi wa vijiji 21 kugomea kupisha hifadhi ya Ruaha.
 
Waziri Nyalandu alisema uamuzi wa kuvihamisha vijiji hivyo ili kupanua hifadhi ya Ruaha ulitokana na tangazo la Rais (GN28) la kuifanya eneo la Ihefu na vijiji vinavyoizunguka kuwa sehemu ya hifadhi.
 
Alisema mgogoro huo ulianza mwaka 2009/2010 baina ya Usangu game reserve na bonde la Ihefu kwenda Ruaha ambapo wakazi wa maeneo hayo ambao walipangwa kuhama walitengewa fidia shilingi Bilion 4 na baadaye kuongezwa Bilion 3 na kuwalipa fidia jumla ya Bilion 7.
 
Alisema baada ya hapo mgogoro ulitokea kwa baadhi ya wananchi kudai kulipwa tofauti na makadirio, wengine kudhurumiwa kabisa  hivyo Serikali imeona wananchi hao wasiondoke kwanza hadi madai yao yahakikiwe kwanza ambapo madai yote yanatarajiwa kuanza kulipwa Julai 1, mwaka huu.
 
Aliongeza kuwa mgogoro huo umetokana na tangazo la serikali kuandaliwa tofauti na matakwa ya wananchi, pia maeneo yalioyoagizwa yakawa tofauti na maeneo yaliyoorodheshwa  ambapo maeneo ya awali hayakuguswa kabisa.
 
Waziri Nyalandu alisema kutokana na hali hiyo, wananchi hao hawataondolewa katika maeneo yao bali timu mbili zimeundwa ili kuchunguza sakata hilo.
 
Alisema timu ya kwanza itafuatilia madai yote kisha watayapeleka kwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya ambaye atayawasilisha wizarani kwa ajili ya utekelezaji.
 
Alisema timu ya pili itakuwa ya wataalamu wa Ikolojia ambao wataangalia mfumo wote wa ekolojia na maji na namna ya kutatua mgogoro ili wananchi wawe sehemu ya hifadhi pamoja na kuangalia namna maji yasiharibu mto Ruaha Mkuu.
 

Aidha alitoa wito kwa Wananchi kuacha kuingiza mifugo yao ndani ya hifadhi ya Ruaha mkuu bali wanapaswa nao kuwa sehemu ya uhifadhi.

No comments:

Post a Comment